Afande Sele afunguka adai hakuna rapper zaidi yake

Rapper wa Morogoro, Afande Sele amesema hadi sasa hajapatikana rapper mbadala wake anayeweza kuifanya hip hop kwa mwelekeo aliokuwa nao yeye.

Amesema amegundua hilo hata kwenye mitandao ya kijamii ambapo licha ya kuongelea vitu vingine, bado mashabiki wanamuuliza kuhusu lini atarejea tena na kudai kuwa hiyo inamaanisha kuwa mbadala haujapatikana.

“Ina maana mpaka sasa hivi hawajapata mbadala, wasanii wengi wanatoka lakini hawana uimbaji wa aina yangu ndio maana wanataka nitoke mimi mwenyewe,” amesema.

Afande ambaye mwaka jana aliingia kwenye siasa na kugombea nafasi ya uongozi kupitia tiketi ya chama cha ACT- Maendeleo, amemweleza mtangazaji wa Jembe FM, JJ kuwa muziki wa sasa umekuwa rahisi sana kuliko zamani.

“Kipindi hiki muziki umekuwa mwepesi watu hawafikiri, hakuna challenge ndio maana watu wanataka wamuone Afande Sele akija upya, wamuone Profesa, wamuone Jay Moe akija upya.”

Afande amedai kuwa kwenye kazi zake zijazo amewashirikisha Linex na Bonta na kwamba ana wimbo uitwao Kisu ambao amepanga kumshirikisha Alikiba.