Askari Mgambo Wavamia Soko Na Kufanya Uharibifu Wa Mali Mkoani Mwanza

Askari mgambo wavamia Soko na kufanya uharibifu wa mali mkoani Mwanza.
Askari mgambo wa manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ambao idadi yao haijafahamika, usiku wa manane wa kuamkia leo ijumaa, wamezua balaa baada ya kuvamia katika soko la matunda la Kirumba na kufanya uharibifu mkubwa wa mali, ikiwemo kuvunja meza, kukata kata ovyo matunda na kuharibu baiskeli hali ambayo imedaiwa kuwasababishia hasara ya mamilioni ya shilingi wafanyabiashara wa soko hilo.
Baadhi ya wafanyabiashara wa matunda, waliofika asubuhi na mapema katika soko hili kwa ajili ya kufungua biashara zao kwa hakika hawakuamini kile walichokuwa wakikiona machoni mwao, huku wengine wakilazimika kuangua kilio baada ya kukuta hali ikiwa tofauti na ile waliyoiacha jana yake.
Kaimu katibu wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Mwanza, Acheni Maulid amefika katika soko hilo kujionea uharibifu wa mali unaodaiwa kufanywa na askari mgambo wa manispaa ya Ilemela, na hapa anatoa msimamo wa chama chake kilichopewa ridhaa na wananchi kuiongoza serikali ya awamu ya tano.
Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga alipotafutwa na ITV ili kuzungumzia tukio hilo, hakutoa ushirikiano wowote na mara zote simu yake ilikuwa ikipokelewa na mtu mwingine ambaye alijibu kuwa yuko kwenye vikao, vikao ambavyo havikujulikana mwisho wake utakuwa ni saa ngapi.
Wafanyabiashara wa soko la kirumba, katika siku za hivi karibuni wamekuwa katika mgogoro mkubwa na uongozi wa manispaa ya Ilemela baada ya kutakiwa kuhamia katika soko la Kiloleli ambalo limejengwa mahususi kwa ajili ya kufanyia biashara ya matunda, lakini swali hapa ni je miundombinu ya soko hilo imekamilika kwa ajili ya wafanyabiashara hao kuhamia ?