Taarifa kutoka Ofisi ya Bunge la Tanzania kuhusu uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EAC).

Uchaguzi wa Wajumbe Tisa (9) watakaoiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) unatarajiwa kufanyika katika Mkutano wa Saba wa Bunge unaotarajiwa kuanza  Aprili 4 mwaka huu.

Uchaguzi huo utakaofanyika Dodoma, utazingatia maisha  ya bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2012 ambalo litafikia ukomo wake Juni 4 mwaka huu.

Taarifa iliyoletwa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Bunge cha Habari, Elimu na Mawasiliano imeeleza kuwa uchaguzi huo utasimamiwa na Katibu wa Bunge ambaye atatoa tangazo kwenye gazeti la serikali la leo.

“Katibu wa Bunge atatoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali kesho( leo ) tarehe 17 Machi, 2017 linaloainisha siku ya uteuzi wa wagombea kuwa tarehe 30 Machi, 2017 saa kumi kamili jioni na siku ya uchaguzi kuwa ni tarehe 4 Aprili, 2017 mara baada ya kipindi cha maswali na majibu Bungeni.” Ilisema taarifa hiyo

Katika taarifa hiyo, msimamizi wa uchaguzi alitoa wito kwa Watanzania wenye sifa za kugombea na kuchaguliwa wajitokeze.
==