CCM Yatoa Onyo kwa makada wake Wanaolalamika Baada ya Kutumbuliwa na Rais

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kukemea vikali kauli zinazotolewa na viongozi au makada wa chama hicho wambao wametenguliwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika nafasi zao mbalimbali walizokuwa wakishikilia.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga aliyasema hayo juzi akizungumza Mjini Iringa katika mkutano na wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyomo mkoani humo ambao ni wananchama na pia viongozi wa chama hicho katika ngazi ya matawi na kata.

Lubinga aliwataka makada hao walioteuliwa na kisha kutemwa na Rais Dkt Mwagufuli ambaye pia ni Mwenyeketi wa CCM Taifa, kuacha kulalamika na kupiga kelele badala yake wakubiliane na mabadiliko hayo kwa nia ya kuheshimu maamuzi ya Ikulu kwa uamuzi uliochukuliwa dhidi yao.

Licha ya kuwa kiongozi huyo hakutaja majina ya viongozi aliowataka kuheshimu maamuzi ya Ikulu, lakini ni dhahiri kuwa miongoni mwa waliolengwa ni Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Moses Nnauye ambaye alitenguliwa katika nafasi yake aliyokuwa ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nafasi aliyoitumikia kwa kipindi cha miezi 15.

Nape alitenguliwa katika nafasi hiyo ikiwa ni saa chache tu tangu alipopokea ripoti ya kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group ambapo ripoti hiyo ilithibitisha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ndiye aliyehusika katika tukio hilo.

Nafasi ya Nape ilichukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison George Mwakyembe ambaye naye nafasi yake ikajazwa na Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Prof. Palamagamba Aidan John Kabudi ambaye ni mbobezi katika taaluma ya sheria.

Mwingine ambaye licha ya kuwa hakuenguliwa na Rais moja kwa moja lakini alionyesha kutoridhishwa na mchakato wa kuenguliwa kwake ndani ya CCM ni aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji. Yeye alienguliwa alipotaka kugombea kwa mara ya pili, na tangu hapo amekuwa akilalamika kwa madai  kuwa njia zilizotumika hazikuwa za haki.

“Rais anapoteua kiongozi na kumpa dhamana ni kwamba anaona kuwa unahitajika, lakini inapofika mahali amekuondoa ujue mazingira yale huwezi kuyamudu na anakuokoa ili usipate laana. Baadhi ya viongozi wameondolewa madarakani, lakini wamebaki wakilalamika mitaani ovyo.”  alisema Kanali Lubinga.

Lubinga alisema kuwa chama hicho sasa kimejikita kuhakikisha kuwa kinarejesha nidhamu na uwajibikaji ndani ya chama na serikali ili viongozi wote waliochaguliwa na kuteuliwa wafanye kazi kwa maslahi mapana ya taifa na wananchi.