JPM - Ole Wake Atakayeingilia Kamati Niliyoiunda,....!!!!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ametoa onyo kali kwa mtu yeyote atakae kwamisha Kamati maalumu aliyoiunda ya  kuchunguza kiwango cha madini yaliyomo kwenye mchanga uliowekwa kwenye makontena.

Amesema kuwa ameamua kuunda kamati hiyo yenye wasomi waliobobea katika masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi ili wawakilishe Watanzania zaidi ya milioni hamsini ambao wanataka kujua ukweli kuhusu rasilimali yao ya madini.

“Nendeni popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa ushirikiano, fungueni makontena popote yalipo, chukuenki sampuli mkazipime mjue kilichomo na naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna anaekwamisha,”amesema Rais Dkt. Magufuli.

Aidha, pamoja na kuunda kamati hiyo, Rais Magufuli amesema kuwa ataunda kamati nyingine ya wachumi na wanasheria kwa ajili ya kufanya tathmini na kuangalia sera na sheria ya madini kwa lengo la kupata taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.

Hata hivyo, ameihakikishia kamati hiyo kutoa ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini ili kufanikisha kazi hiyo na amewataka wawe huru kutumia vitendea kazi wanavyohitaji zikiwemo maabara mbali mbali za taasisi za Serikali na nyinginezo.