Waziri Mkuu Majaliwa apokea taarifa ya mgogoro wa Loliondo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea Taarifa ya Kamati Shirikishi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ya kushughulikia mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye pori tengefu la Loliondo mkoani Arusha, ambapo atatoa maelekezo baada ya kuisoma.

Alipokea taarifa hiyo juzi katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Spika, Bungeni mjini Dodoma. Waziri Mkuu aliiunda kamati hiyo, Desemba mwaka jana mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Kiini cha mgogoro huo ni eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo linagombewa na wawekezaji, wakulima, wawindaji kwa sababu ni mapitio ya wanyama, chanzo cha maji, mazalia ya wanyama, malisho ya mifugo na makazi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Tate William Ole-Nasha, viongozi wa mkoa wa Arusha na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Wengine ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa wa Arusha na wilaya ya Ngorongoro, wawakilishi wa wananchi, wawekezaji na asasi za kiraia ambao wote walishiriki katika uandaaji wa taarifa hiyo.

Waziri Mkuu alisema lengo la kamati hiyo ni kutaka kupata muafaka wa matumizi ya rasilimali zilizoko katika eneo hilo ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake bila ya kuathiri mwingine na kuwezesha wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizoko katika eneo hilo.

“Serikali inataka watu wote tuwe kitu kimoja katika kutunza maeneo yetu, lakini pia shughuli za wananchi nazo ziweze kuendelea ili Watanzania wote tuweze kunufaika na rasilimali zilizoko kwenye maeneo yetu,” alisema.